MBINU ZA USOMAJI VITABU.



Mbinu ya 1: Weka Nia
Jambo la kwanza muhimu ni kuweka nia. Penye nia pana njia. Hivyo, ni muhimu kuanza kuweka nia kuwa unataka kuwa msomaji wa vitabu.

Mbinu ya 2: Tenga Muda
Katika ratiba yako ngumu ya kila siku, tenga muda walau kidogo kwa ajili ya kusoma kitabu. Muda huo unaweza kuwa kuanzia nusu saa na kuendelea kadri ya ratiba zako za kila siku. Unaweza kuamua kuwa ukiamka asubuhi, kabla hujatoka chumbani unatumia nusu saa kusoma. Ama ukiwa kwenye usafiri kwenda kwenye shughuli zako. Ama, usiku kabla ya kulala.
Faida za kutenga muda ni kwamba, usomaji utakuwa sehemu ya ratiba yako ya kila siku. Hivyo, utaiishi.

Mbinu ya 3: Chagua vitabu vinavyokuvutia
Usisome kitabu ilimradi tu kipo. Ukisoma kitabu kisichokuvutia, kinaweza kukuvunja moja ukapoteza mapenzi na vitabu. Chagua vitabu vyenye kuandika mada zinazokuvutia. Binadamu hutofautiana mapendeleo yao. Kuna wanaopenda riwaya za mapenzi, wanaopenda riwaya za kijasusi, wanaopenda vitabu vya hamasa, wanaopenda vitabu vya mafundisho ya dini, wanaopenda vitabu vya kitaaluma.
Kwa mantiki hiyo, kitabu kinachomvutia Maundu, kinaweza kisimvutie Laura; vivyo hivyo cha *Laura* , kinaweza kisimvutie *Hussein* .
Hivyo, ili kuwa na bidii ya usomaji, kuwa mchaguzi wa vitabu.

Mbinu ya 4: Kuwa na marafiki wapenda vitabu
Hili ni muhimu sana. Kuna methali ya Kimarekani isemayo, nioneshe rafiki zako nikwambie wewe ni nani.
Marafiki wana athari kubwa kwenye tabia zetu. Hivyo, pamoja na marafiki wengine kadha wa kadha ulionao, hakikisha pia unao marafiki wanaopenda kusoma vitabu. Hawa watakuchochea hamu ya vitabu kwa sababu mara nyingi mkikutana mtakuwa na mijadala inayohusu vitabu. Lakini pia, watakuwa mahali pa wewe kuazima vitabu vizuri kadri ya matamanio yako.

Mbinu ya 5: Nunua vitabu
Pamoja na matumizi mengi ya kipato chako, tenga kiasi kidogo kwa ajili ya kununua vitabu. Vitabu ni urithi mkubwa sana wa vizazi vyote. Utajiri wa maarifa, hauna kifani chake.
Hivyo, jitahidi kununua vitabu kadri nafasi ya kifedha inapokuruhusu. Hata kama hukisomi leo, kitakufaa kesho. Vitabu vizuri huja na kupotea. Ukivihifadhi, faida ni kwako.

Mbinu ya 6: Jiunge na jamii za vitabu
Hii inaweza kuwa kwa kutembelea na kuwa mwanachama wa Maktaba ama mkahawa wa vitabu. Lakini pia, kwenye ulimwengu huu wa Zama za Habari, kuna makundi mengi ya whatsapp, viber, telegram na facebook ya wasoma vitabu. Jiunge nayo. Huko utapata fursa ya kupata vitabu vingi katika nakala tete.
Vile vile, utashiriki mijadala mbalimbali itakayokuongezea ari ya usomaji

 Mbinu ya 7:
 Beba kitabu kila unapokwenda
Fanya vitabu kuwa sehemu yako kila unapokwenda. Beba kitabu kwenye mkoba wako kila mara. Kuna nyakati utajikuta upo doro kwa dakika nyingi. Ungekuwa na kitabu, zingetosha kufunua kurasa kadhaa.

 Mbinu ya 8:
 Weka orodha ya vitabu vya kusoma
Andika kwenye kijitaftari chako ama kitumizi cha kwenye simu ama ubamba wako orodha ya vitabu unavyokusudia kuvisoma katika kipindi fulani. Inaweza kuwa wiki, mwezi, robo mwaka, nusu mwaka ama mwaka.
Hii itakusaidia kuwa unatiki kila unapokuwa umefikia lengo. Lakini itakupa msukumo kila unapoziona tiki chache kwenye orodha yako.

 Mwisho :
Fanya usomaji vitabu kuwa sehemu ya vipaumbele vyako.

 Storyteller

Dr Cezzane
MBINU ZA USOMAJI VITABU. MBINU ZA USOMAJI VITABU. Reviewed by Maktaba on February 02, 2020 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.