SIMBA NA YANGA

Kitabu:- SIMBA au YANGA? 
Mwandishi:- Hadji Konde

SEHEMU YA KWANZA

Mwandishi anaanza kwa kuzungumzia kauli hii 
ya kwamba Tanzania utani wa Simba na Yanga 
umeongezeka kiasi watu huulizana: "Wewe 
Simba au Yanga" kana kwamba ni lazima kwa 
Mtanzania kuegemea upande mmoja wa timu 
hizi. Shuku hiyo huenda hata kwa viongozi wa 
serikali na Chama (kumbuka kinapochapwa kitabu hiki ilikuwa ni wakati wa Chama Kushika Hatamu(Party Supremacy).

Mwandishi analeta kisa kimoja kwamba kuna 
Kiongozi ingawa hajamtaja jina, alikuwa Mwanakamati wa Yanga. Sasa baada ya 
kuchaguliwa kuwa Kiongozi wa Serikali na Chama, akajiuzulu Yanga. Alihofu kutoa maamuzi juu ya michezo wakati yu mwanakamati wa Yanga. 

Mwandishi anapiga kijembe kwamba haijulikani kama jamaa aliacha "kuipenda" Yanga alipokuwa Kiongozi. 
Anatoa kisa kingine cha Kiongozi kuikana Yanga. 
Inasemwa huyo jamaa alikuwa siku nyingi mwanachama wa Yanga lakini pia wakati fulani 
Afisa wa Chama cha Mpira (FAT, sasa TFF). 

Alipoulizwa kama yu mpenzi wa Yanga alikana kabisa. Lakini ajabu alipoacha kazi FAT na Yanga kuchukua ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati huko Zanzibar Januari 13, 1975 jamaa alifurahia 
mno uhusiano wake na Yanga. 

Tofauti za Simba na Yanga hazikuiacha nyuma siasa kwani kuna visa pia huko. Kimoja wapo ni kile cha Mbunge wa Kigoma Losa Yemba 
(Yawezekana ana unasaba na mwanasiasa Chief 
Lutasola Yemba) Mbunge huyo alisema kuna watu wanadhani Yanga inapenda TANU na Simba kuipinga. Kwani katika bendera ya Simba yenye rangi nyekundu na alama ya Simba ilishabihiana na bendera ya Chama cha African 
National Congress (ANC) kilichopingana na 
TANU katika uchaguzi wa 1962. Lakini kumbe 
hata Kiongozi wa Chama hicho, Zuberi Mtemvu 
alikuwa na kadi ya Yanga. 
Ubishi huo huenda mbali mpaka wapenzi wa timu hizi kutaniana kwa kauli kama " Usicheze 
na Yanga ni klabu ya Serikali". (Hata sasa kabla 
ya utawala huu ilikuwa inasemwa hivi). 

Jambo hili halina ukweli isipokuwa ni kutokana 
na washabiki wa Yanga kuwa na marafiki serikalini na katika TANU. Lakini pia wanachama wa Simba wana marafiki serikalini pia pia Anasisitiza muhimu ni loyalty kwa klabu na kusisitiza uhasama utakuwepo tu. Ilifikia wakati watu waliomba serikali izifute klabu zote mbili lakini ikaonekana haitakuwa suluhisho. 
Wanachama hao watajiunga na kujiita majina 
mengine kama Yanga ilivyopitia "Jangwani", 
"Navigation", "Taliana" na "New Young's" 

Mwandishi anasisitiza umuhimu wa uhasama 
wa washabiki na wanachama wa klabu hizi kuwa haufai. Kwamba ni vema wakaongozwa na akili timamu wakati wote. Ikiwa mmoja amefungwa akubali kimchezo na sio kuwa na 
chuki. 

Sehemu Ya Pili.

WACHEZAJI WANA UHASAMA?

Uhasama nje ya uwanja ni tofauti na uwanjani.
Wakati Wapenzi na wanachama wa klabu hizi
wakiapizana na pia kukasirika pindi timu zao zinaposemwa vibaya, wachezaji wao wala
hawana habari. Wao hutaniana kirafiki bila ya kuonesha uhasama.

Hawa huwa pamoja kwenye timu zao za mikoa na timu ya Taifa (kombe la mikoa limefutwa ila miaka michache
iliyopita liliibuka na kisha kufa) ila hali hiyo ya urafiki imekuja karibuni kwani
kumbe hata pasi ndani ya timu ya Taifa zilikuwa za kitimu kwamba akifunga mchezaji wa Yanga
basi ushindi ni wa Yanga. Vivyo hivyo akifunga
wa Simba ni ushindi wa Simba. Hali hii ilisababisha Tanganyika kushindwa kombe la Gossage (Brand moja ya sabuni chini ya
Unilever) na ndiyo mwanzo wa CECAFA Challenge Cup. Hii ni pamoja na Tanganyika
kuwa na timu nzuri kuliko nyingine. Kombe hilo lilikuwa miaka 3 baada ya Tanganyika kuwa huru. Lakini mwaka 1975 uhasama ukapungua. Baada ya Yanga kuchukua ubingwa Zanzibar, wachezaji wa timu zote walijumuika na kunywa na kucheza pamoja.

Mchezaji wa Yanga, Muhidini Fadhili alizungumza na Haidari (Abeid?) naye Haidari akasema: "Leo siku yako
nicheke, nami nilipokuwa bingwa nilipata nafasi
ya kukucheka". Wote wakacheka na kuendelea
na starehe.

Mwandishi anahitimisha kwa kusema jambo baya ni kwamba wachezaji wa timu hizi mbili, hutilia maanani mechi zao kuliko na timu
nyingine. Anasisitiza kuwa yeye anapenda utani unaoendeleza mchezo wa mpira na si kulogana
(kuna ukweli hapa hata sasa).
SIMBA NA YANGA SIMBA NA YANGA Reviewed by Maktaba on September 08, 2017 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.