BURIANI PROFESA EUPHRASE KEZILAHABI


LEO ASUBUHI, nimekutana na ujumbe kwenye kundi-sogozi la wasoma vitabu, ya kwamba, miongoni mwa magwiji katika Fasihi ya Kiswahili, amefariki dunia.  Namzungumzia Profesa Euphrase Kezilahabi.  Profesa huyu aliyekuwa akifundisha Chuo Kikuu nchini Botswana, ameelezewa na wanazuoni wengi kuwa ndiye mrithi hasa wa Gwiji wa Kiswahili kupata kutokea, Sheikh Shaaban Robert.

Mimi, nimekuwa mwanafunzi wa Profesa Kezilahabi tangu mwaka 1997, nilipomsoma kwa mara ya kwanza, nikiwa ndiyo ninaanza Kidato cha Kwanza, pale Njombe Sekondari.  Wenyewe tukiita NJOSS.  Nilikutana na vitabu vyake viwili nikiwa maktaba shuleni hapo.  Vitabu hivyo, Nagona na Mzingile, vilikuwa vigumu sana kwangu.  Lakini, vilinivutia kuvisoma.  Nikajikuta, hadi leo hii, nimemsoma kwenye vitabu vyake vyote alivyowahi kuvichapa.  Ingawa, sijahitimu uanafunzi juu yake, ninaona fahari kwamba, lugha yetu adhimu ya Kiswahili, imebahatika kuwa na Profesa Euphrase Kezilahabi, kama miongoni mwa mafundi wake.

Profesa Euphrase Kezilahabi ni nani?
Alizaliwa Aprili 13, 1944 kijijini Namagondo, ndani ya kisiwa cha Ukerewe.  Kisiwa hicho kimo ndani ya Ziwa Victoria.  Alipata Shahada ya Ualimu na Fasihi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.  Miongoni mwa shule alizopata kufundisha baada ya kuhitimu kwake, ilikuwa Mkwawa High School (nimebahatika kusoma shule hii), mkoani Iringa.  Alifundisha kipindi kifupi tu, akarejea UDSM kusoma Shahada ya Umahiri.  Jambo la kipekee, wakati akisoma shahada ya umahiri, tasnifu yake ilihusu riwaya za Shaaban Robert.  Na hata alipokwenda Marekani kusoma Shahada ya Uzamifu, aliandika tasnifu kuhusu 'African Philosophy and the Problem of Literary Interpretation'.

Tasnifu hiyo, ni kielelezo cha wazi juu ya falsafa yake ya Kiafrika juu ya maisha.  Vilevile, kazi zake za kifasihi, wakati wote wa maisha yake, zilijikita kwenye Falsafa ya Maisha.

Miongoni mwa vitabu vyake maarufu vya riwaya ni Rosa Mistika.  Profesa Kezilahabi alikiandika kitabu hiki mwaka 1976.  Nilibahatika kukisoma nikiwa Njombe Sekondari.  Kwangu, kinabaki kuwa miongoni mwa vitabu bora kuwahi kuandikwa katika Kiswahili.  Ndiyo maana, kwenye riwaya yangu mpya ya RAFU, ambayo inatarajiwa kutoka hivi karibuni, nimeitumia riwaya hii kuufikisha ujumbe muhimu kwa mhusika mkuu wa riwaya hiyo.  Tukiachana na hayo, riwaya hii imegusia masuala mazito katika jamii kama utoaji mimba kwa wasichana wadogo, mapenzi katika umri mdogo na ukosefu wa maadili kwa viongozi katika jamii.

Mchambuzi Roberto Gaudioso alipata kuandika kuwa: "Euphrase Kezilahabi aliandika tasnifu ya uzamivu kuhusu falsafa ya Kiafrika na fasili ya fasihi mwaka 1985, yaani katika muda ambapo aliandika diwani ya Karibu Ndani (1988) na riwaya za Nagona (1990) na Mzingile (1991). Sifa ya kazi hizi ni falsafa yake inayoonyeshwa kwa sitiari na mafumbo mbalimbali. Mafumbo haya yanaweza kueleweka tukisoma tasnifu yake kuhusu falsafa. Zaidi ya hayo, tasnifu hiyo inasaidia sana kuelewa falsafa yake kwa jumla."

Kazi yake nyingine yenye kusisimua ni Kichwa Maji aliyoichapisha mwaka 1974.  Kwenye riwaya hii, ndimo nilipojifunza falsafa ya maisha kwamba, chuki haina nguvu kama unayemchukia anakupenda.  Fundi huyu wa Fasihi ya Kiswahili amegusa namna binadamu anavyokumbana na mahangaiko, taabu, bughudha na karaha ndani ya jamii yake.  Kuna matumizi mabaya ya madaraka vile vile.  Ni miongoni mwa riwaya bora za kisasa.

Kama nilivyopata kuandika mara nyingi, lugha ya Kiswahili imebahatika.  Miongoni mwa bahati hizo ni kuwahi kuwepo kwa gwiji Profesa Euphrase Kezilahabi.  Kwenye riwaya yake ya Dunia Uwanja wa Fujo aliyoitoa mwaka 1975 alielezea falsafa ya maisha ya namna ambavyo kila mtu huja duniani kufanya fujo zake.  Si hivyo tu, bali pia, kuiletea jamii yake madhila kama mauaji, ukabila, umalaya, ubakaji, ulevi kupindukia, uchawi na kila aina ya fujo na karaha.  Tukiitazama falsafa ya maisha kupitia kazi hii, tunakubaliana kwamba, matendo ya wanadamu yamejaa fujo, na unafiki.  Ndiyo maana, hata mwaka 1979 alipotusimulia kupitia riwaya ya Gamba la Nyoka, gwiji huyu alijenga taswira kwa uwezo mkubwa ili kuibua hisia kali miongoni mwa wasomaji.  Lengo lake likiwa, kuzichokonoa fikra za msomaji, ziweze kuupembua vema unafiki katika matendo ya wanadamu.

Profesa Euphrase Kezilahabi ni fundi hasa.  Pamoja na kuwa Kiswahili hakikuwa lugha yake ya kwanza, lugha yake ya kwanza ilikuwa Kikerewe, bado, amekitendea haki vilivyo.  Ukiachia mbali riwaya, gwiji huyu aliandika tamthiliya ya Kaptula la Marx mwaka 1978 akielezea namna kaptula la mwanafalsafa Karl Marx lilivyotupwaya kupitia sera zetu za Ujamaa.

Nguli huyu ni mshairi pia.  Aliandika Kichomi (1974) na Karibu Ndani mwaka 1988.  Kama alivyopata kuandika mchambuzi na mwanazuoni wa Fasihi, Roberto Guadioso, ili kumwelewa vema, yakupata kuelewa falsafa za Kimagharibi, na vilevile falsafa za Kiafrika juu ya maisha.  Lakini, ukiyasoma mashairi kwenye vitabu hivi, ni rahisi zaidi hata kuzielewa riwaya zake za Nagona na Mzingile.

Kwa maelezo hayo, unaweza kupata woga na kudhani kazi zake ni ngumu kiasi cha kutosomeka.  La hasha.  Aliandika kazi akiyatazama mazingira haya haya ya Kiafrika.  Aliiangazia jamii yake.  Mifano ya wazi unaweza kuiona kwenye riwaya za Rosa Mistika na Karibu Ndani.  Yaliyoandikwa, ni mambo yenye kutukia katika jamii zetu.  Isipokuwa, aliandika akiyaangazia kwa jicho la tatu, ambalo ni, Falsafa ya Kiafrika juu ya Maisha.

Mbuyu katika fasihi umeanguka.  Profesa Euphrase Kezilahabi alikuwa fundi wa lugha za kifasaha na zenye kunyooka, huku zikiangazia mambo nyeti.

Ni wazi, lugha yetu adhimu, ambayo ni tamu kama titi la mama, imebahatika sana.  Moja ya bahati hizo, ni kupata kuwa na Profesa Euphrase Kezilahabi, kama mwanazuoni wake.

Nimalizie taabini yangu, kwa kumwandikia nguli huyu shairi, japo kwa beti chache:

Nimesikia habari, Kezilahabi hayupo,
Kaenda yake safari, usorudi uendapo,
Ila kaacha fahari, urithiwe ungalipo,
Buriani wetu fundi, umenururisha lugha.

Buriani wetu fundi, ulonururisha lugha,
Juu zaidi ya shundi, pasi kurusha mabega,
Kirefu chake kilindi, pasipo singe kutoga,
Buriani eh Mwalimu, mwalimu wetu mahiri.

Buriani eh Mwalimu, ulojawa umahiri,
Kuipa lugha utamu, riwaya na ushairi,
Uliongezea hamu, Kiswahili kushamiri,
Buriani eh Mwandishi, mwandishi pasi kuchoka.

Buriani eh Mwandishi, hukuchoka kuandika,
Riwayazo fikirishi, akili ikatumika,
Ziloukuza utashi, fikira kuimarika,
Buriani eh rafiki, kupitia Kiswahili.

Buriani eh rafiki, fundi kwenye Kiswahili,
Kazizo 'zimithiliki, kwa halua na hamali,
Ufundi haupimiki, kwa mizani na jedwali,
Buriani ndugu yetu, ulale pahala pema.

Natoka pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa nguli huyu.  Zaidi, kwa jamii nzima ya wazungumzaji wa Kiswahili, ambao, kwa hakika, tumempoteza fundi.

Nakuombea pumziko la amani, Profesa Euphrase Kezilahabi.

Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Alhamini, Januari 9, 2020
BURIANI PROFESA EUPHRASE KEZILAHABI BURIANI PROFESA EUPHRASE KEZILAHABI Reviewed by Maktaba on January 12, 2020 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.